Pages

Tuesday 13 March 2012

CHANGUDOA NDO ALIYE MLIZA WAZIRI.


WIZI kwenye chumba cha Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Kighoma Malima (pichani) mwishoni mwa wiki iliyopita katika Hoteli ya Nashera mkoani Morogoro, umedaiwa kufanywa na mwanamke anayejiuza, maarufu kama changudoa.

Vyanzo vyetu mbalimbali mjini Morogoro vimedai kuwa mwanamke huyo siku hiyo ya tukio alionekana maeneo ya hoteli hiyo ambapo inadaiwa aliweza kuagiza soda na kunywa kisha kuondoka hotelini hapo na baada ya muda mfupi alirejea.

Habari zinasema, mwanamke huyo haikujulikana aliondokaje katika hoteli hiyo, hivyo watu kumlenga yeye kuwa ndiye mwizi baada ya habari za naibu waziri kuibiwa fedha na mali mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 23 kuzagaa.

Mpasha habari wetu mmoja amedai kuwa mwanamke huyo ambaye amekuwa akihusishwa na wizi pamoja na utapeli mbalimbali mkoani hapa, amekuwa akionekana katika baadhi ya hoteli kubwa.

“Kuna jamaa yangu amewahi kuibiwa katika hoteli moja na mwanamke huyo tunayedhani kuwa kamuibia Waziri Malima.Inasemekana ana ‘funguo malaya’ na hata dawa ya usingizi.
“Siku aliyoibiwa jamaa yangu mwanamke huyo aliingia katika chumba chake akajifanya kuomba simu, baadaye jamaa yangu akajikuta amelala fofofo, akakombwa kila kitu. “Nadhani alitumia dawa ya usingizi, sasa sijui mazingira ya chumba na hoteli aliyolala naibu waziri yalikuwaje,” kilisema chanzo hicho.

Wajihi wa mwanamke huyo ambaye inadaiwa ana kundi la uhalifu ambalo hudiriki kuvunja sehemu wanayodhani ina mali au fedha, ni mweupe, mrefu, ana umbo mithili ya wanawake wa Kitutsi, juu mwembamba, chini mnene na inasemekana hupendelea kutembelea pia jijini Dar es Salaam na Mwanza.

Mwandishi wetu alizungumza na mlinzi mmoja wa Hoteli ya Nashera na kumuuliza kama alimuona mwanamke yeyote siku hiyo ya tukio hotelini hapo ‘akimzengea’ waziri lakini akakataa kuzungumzia suala hilo.

Aidha, Naibu Waziri Malima alipozungumza na gazeti hili alisema hamjui mtu aliyemuibia na hakuwahi ‘kuzengewa’ na mwanamke yeyote siku hiyo.

ALIYEIBA ALIKUWA PEKUPEKU
Naye Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Morogoro (RCO), Hamisi Selemani ambaye siku ya tukio alikuwa akikaimu nafasi ya kamanda wa mkoa, alisema uchunguzi wao wa awali ulibaini kuwa aliyeiba hakuwa amevaa viatu, yaani alikuwa pekupeku.
“Nyayo za mtu huyo zilionekana nje ya chumba namba 125 alichokuwa amelala naibu waziri,” alisema Kamanda Selemani.

ALICHOSEMA RPC
Alipoulizwa juzi na gazeti hili juu ya changudoa huyo anayedaiwa kufanya tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, (RPC) Adolfina Chialo alisema hajajua kama changudoa huyo anahusika lakini akakiri kuwa tayari watu watano wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
“Kuna vitu vya Naibu Waziri Malima vimepatikana isipokuwa fedha lakini tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo,” alisema.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Maneno Juma (25),  Juma Athumani (23) ambao ni wakazi wa Chamwino, Kwa Mgulasi, Ramadhani Athumani (24) na  Abdallah Hassan (25) wakazi wa Mafiga.
Kamanda alimtaja mwanamke Halima Ramadhani (37),  mkazi wa Kichangani Morogoro ambaye alisema  alikutwa na simu tatu  na Kompyuta mpakato (Lap Top), mali za  Naibu Waziri Malima.

MALI ALIZOIBIWA
“Tumefanikiwa kukamata mali za waziri kwa asilimia 90 nikimaanisha kwamba  vitu vyote vimepatikana isipokuwa fedha,” alisema Kamanda Chialo bila kufafanua zaidi.
Malima alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kubembelezwa kwa saa tano, alitaja mali alizoibiwa na thamani yake katika mabano kuwa ni Kompyuta mpakato tatu aina ya Dell (Sh. Milioni 5.6), Digital Recoder mbili na head phone zake (Sh. Milioni 1), simu tatu aina ya Nokia S6 ( Sh. 500,000),  Nokia E200 (Sh. 250,000) na Blackberry ambayo hakutaja thamani yake.

Vingine ni pete mbili za madini ya fedha, fedha taslimu Dola za Kimarekani 4,000 (Zaidi ya shilingi milioni 6.3), shilingi milioni 1.5, kadi mbili za benki, mabegi matatu ya nguo na nyaraka mbalimbali za serikali, zote zikiwa na thamani ya jumla ya shilingi milioni 23.25.

Source: GPL

2 comments:

Anonymous said...

Ingekuwa nchi za watu angejiuzuru kwa kuwa mzembe!!

Anonymous said...

sioni uzembe badokwani hawakusema kama alikuwa na changudua,pili kama huyo changu anafunguo bandia,bado ulinzi wa hotelini una utata