Pages

Thursday 15 March 2012

TANAPA 'YALIWA' KWENYE MAGOGO YA MITIKI.



ZAIDI ya Sh bilioni 3 ziko hatarini kupotea baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kuingia mkataba wa kuvuna miti aina ya mitiki yenye thamani ya Sh bilioni 4 na 5, huku yenyewe ikiambulia Sh bilioni 1.3. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, alisema hayo juzi baada ya kusomewa taarifa iliyoonesha kuwapo kampuni iliyopewa zabuni ya uvunaji mitiki katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Morogoro. 

Katika taarifa hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Vitalis Uruka, alisema Tanapa makao makuu ilitangaza zabuni kwa wazi akapatikana mshindi aliyepewa kazi ya kuvuna mitiki hiyo na kulilipa shirika hilo Sh bilioni 1.3. 

Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Paul Banga, alisema mzabuni huyo anatakiwa kuvuna meta za ujazo 6,437. 737 za mitiki sawa na miti hiyo 6,383 na hadi sasa ameshavuna meta za ujazo 1,155 sawa na miti 1,935. Kwa mujibu wa Banga, kutokana na zabuni hiyo, mzabuni aliilipa Tanapa Sh bilioni 1.37. 

Aliongeza kuwa mitiki hiyo ilipandwa na wataalamu wa Idara ya Misitu na Nyuki mwishoni mwa miaka ya 1950 hadi mwanzoni mwa mwaka 1960 kabla ya eneo hilo kupandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Taifa mwaka 1992. 

Baada ya kupata taarifa hizo, Maige alisema kwa bei ya sasa katika soko la kimataifa meta moja ya ujazo jijini Mumbay, India ni dola 800 za Marekani wakati katika soko la Madrid, Hispania ni dola 1,200. 

Alisema iwapo mauzo ya meta za ujazo 6,437 yangefanyika kwa bei za sasa, Tanapa ingejipatia Sh bilioni 4 hadi 5 tofauti na malipo yaliyofanyika ya Sh bilioni 1.3. 

“Hapa sisemi yametafunwa mamilioni ya fedha kupitia zabuni ya kifisadi, sitaki kusema hayo, ila muwe waangalifu sana katika maeneo haya ambayo hamna utaalamu nayo. 

“Kiwango hiki shirika limepunjwa … ingawa zabuni ilikuwa ni ya wazi, tayari mmeshaingia mkataba, sitaki niwaanzishie vurugu, bali bado kuna haja ya kukutana na mhusika ili kuingia kwenye majadiliano mapya yatakayofikia uamuzi wa kubadilisha bei. 

“Nashauri katika maeneo haya ambayo hamna utaalamu nayo yakiwamo ya misitu, ni vyema mkashirikiana na watu wa Idara ya Misitu na Nyuki, ndio wanajua bei halisi ya mitiki,“ alisema Waziri Maige. 

Watanzania wachangamke Akiwa Iringa, Maige aliwataka Watanzania wabadili fikra za uwekezaji kwa kuwekeza katika sekta ya mazao ya misitu badala ya nyumba na mifugo, kwa kuwa sekta hiyo ina faida kubwa ambayo si rahisi kuonwa na watu wasiojua kukokotoa faida za kibiashara. 

Maige alisema wakati mahitaji ya mbao nchini kwa mwaka yanafikia meta za mraba milioni tano, uwezo wa mashamba yaliyopo ni kuzalisha meta za mraba milioni 1.5 tu. Alisema Sh milioni 40 zinatosha kuhudumia ekari moja ya shamba la mitiki kwa miaka 20, lakini mazao yake yakazalisha zaidi ya Sh bilioni 3. 

“Lakini ukijenga nyumba ya kupangisha kwa Sh milioni 40 hiyo hiyo, inaweza kukuchukua miaka hiyo au zaidi kurudisha kiasi ulichotumia kwa ujenzi wake,” alisema. Alisema nyuki ni eneo la pili katika sekta ya misitu lenye faida kubwa ambayo si rahisi kuonekana kwa hesabu za kawaida. 

Alifafanua kuwa kwa wastani mzinga wa kisasa wa nyuki unatoa lita 40 za asali kwa mwaka huku lita moja ikiuzwa Sh 10,000 ambayo inafanya jumla ya mapato ya mzinga mmoja kwa mwaka yawe Sh 400,000. 

Kwa mujibu wa Maige, katika ekari moja ya msitu, kitaalamu mfugaji anaweza kuweka mizinga 3,000 ambayo kwa hesabu ya mwaka inazalisha Sh bilioni 1.2. Alisema nyuki wana faida kuliko ng’ombe, kwa kuwa ng'ombe mmoja anayefugwa vizuri na kwa gharama kubwa, kwa miaka mitano anaweza kuuzwa kwa kati ya Sh 300,000 na Sh 400,000 sawa na mapato ya mzinga mmoja kwa mwaka. Imeandikwa na John Nditi, Kilombero na Frank Leonard, Iringa.

No comments: