Pages

Tuesday 27 March 2012

KULIKONI MAGUFULI?


NA DUNSTAN SHEKIDELI (Mwandishi wa GPL), MOROGORO
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli wiki iliyopita akiwa mjini hapa alitoa kali ya mwaka baada ya kukataa kukalia kiti alichoandaliwa mkutanoni, hali iliyozusha minong’ono kutoka kwa watumishi wa serikali kuwa sumu inamtesa.

Katika tukio hilo lililowaacha midomo wazi wafanyakazi wa wizara yake wa mkoani hapa na  mwandishi wetu kujionea, Dk. Magufuli baada ya kugoma kukalia kiti alichoandaliwa na wenyeji wake, alichukua kiti alichoandaliwa mwenyeji wake, Mkuu wa Chuo cha Ujenzi, Injinia Mdee na kukikalia.

 Ajabu kubwa ni kwamba kiti hicho cha Magufuli baada ya kukikataa,  hakuna kiongozi mwingine aliyekubali kukikalia na badala yake kikashushwa chini ya jukwaa na kubaki wazi hadi mwisho wa mkutano.

Mbali na kugoma kukalia kiti hicho mbele ya wafanyakazi wa idara zote za Wizara ya Ujenzi mkoani hapa waliofika katika  Ukumbi wa Chuo Cha Ujenzi mjini hapa kumsikiliza, Dk. Magufuli pia hakunywa maji ya chupa yaliyokuwa meza kuu.


Kama vile hiyo haitoshi, waziri huyo pia aliandaliwa chakula cha mchana ambapo kwa mshangao wa wengi, alikataa  kula bila wafanyakazi kuelezwa sababu ya kiongozi wao kukataa mlo huo.

Minong’ono iliyoenea katika ukumbi huo ni kwamba kitendo hicho cha Magufuli kususa vitu hivyo hadharani ni hofu ya sumu hasa ikitiliwa maanani kwamba Naibu wake, Dk. Harrison Mwakyembe amekuwa akiteseka kwa ugonjwa kipindi kirefu hadi akapelekwa India Oktoba 9 mwaka jana kwa matibabu kutokana na kile kilichodaiwa kuwa alilishwa sumu katika moja ya mikutano yake ya kikazi.

Mwandishi wetu alimfuta Waziri Magufuli kwa lengo la kupata ufafanuzi wa kukataa kiti, maji na chakula alichoandaliwa ambapo alipotakiwa kujibu maswali hayo, aligoma kufafanua na kujibu kwa mkato:
“Samahani kijana nimechelewa sana, nina mkutano sehemu nyingine, hivyo sitakuwa na muda wa kuzungumza na wewe. Nisamehe kwa hilo.”


Katika mkutano huo, Dk. Magufuli pamoja na mambo mengine, aliwataka watumishi hasa wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuacha kula rushwa na akasema atatumia maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa nchini (Takukuru) na jeshi la polisi kuwakamata wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Injinia Doroth Mtenga alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo la bosi wake kugoma kukalia kiti na kula chakula walichomuandalia naye alionekana kukwepa kuzungumzia hilo akasema:
“Mimi sijui ni kwa nini amekataa na kwamba siwezi kuzungumzia chochote kuhusiana na hilo.”

Afisa mmoja wa wanakamati ya maandalizi ya mkutano huo aliyeomba hifandhi ya jina lake kwakuwa siyo msemaji wa Tanroads, alisema anadhani waziri amefanya hivyo kwa sababu ya mambo ya kiusalama.
“Wakati tunambadilishia kiti alisema eti ni kirefu lakini kiukweli ni kwa sababu za kiusalama … kuna kitu amehofia ndiyo maana hata chakula amekataa kula, hili ni tukio la mwaka.”

Baadaye mwandishi wetu alibaini kuwa Waziri Magufuli alikwenda hoteli aliyofikia iitwayo Nashera, ile ambayo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima ‘alilizwa’ mamilioni ya shilingi na vitu kadhaa vya thamani hivi karibuni.

No comments: