Pages

Thursday, 15 March 2012

HOSPITALI YA BEREGA YAANZA KUTENGENEZA DRIPU.


HOSPITALI ya Berega iliyopo wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, inatarajia kuondokana na tatizo la uhaba wa maji ya mishipa ‘ dripu’ baada ya kukamilika kwa kituo cha kutengeneza maji hayo .


Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Mchungaji Isaack Mgego, alisema ili kufanikisha mpango huo, wamejenga matangi ya kuhifadhi maji ya mvua yanayovunwa na baadaye kusafishwa kwa kutumia mashine maalumu na kupata maji hayo.

Alisema , mpango huo una lengo la kukabiliana na changamoto za hospitali hiyo ambayo inamilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro ikiwa ni mojawapo ya hospitali inayowahudumia watu wengi wa Wilaya ya Kilosa na nje ya wilaya hiyo.

" Tunapokea wagonjwa wengi wa nje kutoka vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Kilosa na wengine nje ya wilaya, pia huduma za majeruhi wanaopatwa na ajali za magari kwenye barabara kuu ya Morogoro- Dodoma, hivyo kituo hiki kitatusaidia kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji ya mishipa" alisema Mkurugenzi wa Hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo , kukosekana kwa maji hayo mara kwa mara kunaiweka hospitali hiyo kwenye wakati mgumu , na hivyo uongozi umefikia uamuzi wa kujenga kituo hicho cha kutengeneza maji ya mishipa.

“ Tumeamua kujenga kituo cha kutengeneza maji ya mishipa , tumejenga matangi ya maji ambayo yanavunwa , ni mahususi kwa ajili ya kutengeneza maji ya mishipa ili kuondokana na changamoto hizi,” alisema Mkurugenzi wa Hospitali hiyo.

Alisema, Kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kutengeneza dripu za maji ya mishipa kuanzia 200 hadi 300 kwa mwezi, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa gharama ya uagizaji wa maji hayo kutoka nje.

Hospitali hiyo ina vitanda 140 kati ya hivyo vilivyosajiliwa na Serikali kuweza kupata ruzuku ni vitanda 120 , ambapo wastani wa wagonjwa wa nje wanaofika kutibiwa ni kati ya 100 hadi 150.


Source: Habari leo

No comments: