Pages

Showing posts with label Habari za Biashara na Uchumi. Show all posts
Showing posts with label Habari za Biashara na Uchumi. Show all posts

Thursday, 5 April 2012

MACHINGA WATAKIWA KUHAMIA KIKUNDI.


UONGOZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro umewataka wafanyabaishara ndogondogo kutumia Soko la Kikundi badala ya kupanga bidhaa zao chini maeneo ya barabarani. 

Naibu meya wa manispaa hiyo, Lidya Mbiaji, alisema wafanyabiashara hao wamekithiri mjini hapa kwa kufanya biashara hususan nyakati za jioni barabara za Madaraka, mzunguko wa daladala maeneo ambayo yamepigwa marufuku kwa biashara.

“Wafanyabishara wote wanatakiwa kufanya shughuli zao eneo husika la Kikundi, ili kupisha mji kuwa safi na salama kwani wanapofanya hivi mandhari ya mji yanakuwa siyo nzuri” alisema Mbiaji."

Mbiaji alisema maeneo hayo ya barabara waliyokuwa wakiyatumia ni hatari kwa maisha yao na hata afya za walaji, kwani wamekuwa wakipanga bidhaa chini.

Pia, alisema soko la Kikundi ndilo limeandaliwa kwa wafanyabishara hao na kwamba, tayari halmashuri imeshaboresha kwa kuweka taa na huduma zingine.

Alisema halmashauri hiyo inaendelea na kuboresha soko hilo liweze kukidhi mahitaji yote ya wafanyabiashara hao.

Thursday, 15 March 2012

WANAWAKE 980 WAPATIWA MAFUNZO NA USHAURI JUU YA UJASIRIAMALI.


JUMLA ya wanawake 980 mkoani Morogoro wamepatiwa mafunzo na ushauri juu ya kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, ikiwa ni pamoja na kupewa uwezo wa kisheria kupitia dirisha la upashanaji habari la wanawake mkoani hapa. 

Hayo yamesemwa na Ofisa wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wa Manispaa ya Morogoro, Monica Lindi wakati alipokuwa anasoma risala katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Jamhuri, mkoani hapa. 

Lindi alisema kuwa Halmashauri katika manispaa ya Morogoro wameamua kuwa na dirisha la upashanaji habari la wanawake ambalo litawasaidia wanawake kupatiwa ushauri ikiwa ni pamoja na ufadhili hivyo kujiendeleza na kujikwamua kiuchumi. 

Aidha alisema kuwa pamoja na mafanikio walioyapata lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama upungufu wa mabweni na hosteli kwa watoto wa kike katika shule za serikali katika manispaa hiyo. 

Changamoto nyingine ni jamii kukosa hamasa za kuchangia katika elimu hasa kwa watoto wa kike na kuchangia shughuli za sherehe na hivyo kuacha jukumu la kumwendeleza mtoto wa kike kwa wafadhili na serikali. 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Halima Dendegu akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa alisema kuwa jamii inapaswa kutambua umuhimu wa kuwawezesha wasichana kupata elimu bora ambayo itawawezesha kupata ajira na hivyo kuongeza kipato kwa jamii na taifa kwa ujumla

SEREKALI KUFUTA LESENI ZA UCHIMABjI MADINI.

Naibu waziri wa Nishati na Mdini Mh. Adam Malima
---
WIZARA ya Nishati na Madini imesema, njia moja wapo ya kuondoa migogoro kwenye sekta ya Madini ni kutathimini upya leseni ambazo zimetolewa kiholela kwa lengo la kubaini ‘madalali’. 

Hatua hiyo inatarajia kuanza kutekelezwa wakati wowote kuanzia sasa kwa kutumia wataalamu wake. 

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima wakati akizungumzia migogoro katika sekta hiyo inayogusa watu waliopewa maeneo makubwa ya kufanya utafiti na uchimbaji kisha wakashindwa kutimiza masharti kwa muda mrefu. 

Naibu waziri huyo alisema hoja ya kuzipitia upya leseni zote zilizotolewa na Maofisa wa Madini wa Mikoa na Kanda kwa wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo ambazo zimeshindwa kufanya kazi kulingana na masharti ya uendeshaji wa Sekta ya uchimbaji wa madini nchini na hivyo kusababisha migogoro ya kimaslahi baina ya wananchi na wenye madini. 

Naibu Waziri huyo, alitoa msimamo wa Wizara yake tarehe 7 march 2012 mjini hapa wakati akizungunza na Wadau wa Sekta ya Madini wa Mkoa wa Morogoro, kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, baada ya kutembelea Tarafa ya Mkuyuni na Matombo ambazo baadhi ya vijiji vyake kuna shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbalimbali. 

“Tatizo la madini kwa Mkoa wa Morogoro si la leo, bali ni la siku nyingi na yana sura nyingi, yapo matatizo Kilosa, Mahenge na Morogoro vijijini, yapo ya sura ya wachimbaji, mfumo wenyewe na kuanzia sasa Serikali inayatafutia majawabu ya kudumu,” alisema Naibu Waziri wa Madini. 

TANAPA 'YALIWA' KWENYE MAGOGO YA MITIKI.



ZAIDI ya Sh bilioni 3 ziko hatarini kupotea baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kuingia mkataba wa kuvuna miti aina ya mitiki yenye thamani ya Sh bilioni 4 na 5, huku yenyewe ikiambulia Sh bilioni 1.3. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, alisema hayo juzi baada ya kusomewa taarifa iliyoonesha kuwapo kampuni iliyopewa zabuni ya uvunaji mitiki katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Morogoro. 

Katika taarifa hiyo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Vitalis Uruka, alisema Tanapa makao makuu ilitangaza zabuni kwa wazi akapatikana mshindi aliyepewa kazi ya kuvuna mitiki hiyo na kulilipa shirika hilo Sh bilioni 1.3. 

Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Paul Banga, alisema mzabuni huyo anatakiwa kuvuna meta za ujazo 6,437. 737 za mitiki sawa na miti hiyo 6,383 na hadi sasa ameshavuna meta za ujazo 1,155 sawa na miti 1,935. Kwa mujibu wa Banga, kutokana na zabuni hiyo, mzabuni aliilipa Tanapa Sh bilioni 1.37.