Pages

Thursday, 15 March 2012

MOROGORO WAFANYA KWELI UENYEJI LIGI DARAJA LA KWANZA.


CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) kimetuma kiasi cha Sh milioni 10 
kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ( TFF) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa masharti ya kulipa Sh milioni 25 ili kuwa mwenyeji wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza zinazotarajia kuanza Machi 31. 

Katibu Mkuu wa MRFA, Hamis Semka, amesema mjini hapa kuwa Mkoa wa Morogoro 
umetuma kiasi cha Sh milioni 10 na kilichobakia kitakamilishwa ndani ya muda uliopangwa ikiwa ni sehemu ya kukamilisha masharti ya TFF baada ya kutuma maombi yao. 

Lakini alisema Mkoa wa Morogoro mbali na kukamilisha kiwango cha fedha, pia una mazingira mazuri ya kuwezesha kuchezwa kwa fainali hizo bila kuwa na matatizo yoyote hasa kulingana na historia ya kuwa Mkoa wa Kimichezo. 

Kwa mujibu wa TFF , baadhi ya mikoa ambayo imeshatuma maombi ya kuwa mwenyeji wa 
fainali hizo ni Mbeya, Morogoro, Mwanza, Ruvuma na Tabora. 

Hata hivyo, Kamati ya Ligi itatangaza kituo cha fainali hizo baada ya Machi 15 mwaka huu 
ambayo ni siku ya mwisho kupokea maombi na kutimiza masharti yaliyowekwa. 

Timu zilizofuzu kucheza hatua ya fainali kutoka kundi A ni Polisi ya Dar es Salaam, Mgambo 
Shooting ya Tanga na Transit Camp ya Dar es Salaam, Kundi B ni Mbeya City Council, Mlale 
JKT ya Ruvuma na Tanzania Prisons ya Mbeya wakati Kundi C ni Polisi ya Tabora, Polisi ya 
Morogoro na Rhino Rangers ya Tabora.

No comments: