JUMLA ya wanawake 980 mkoani Morogoro wamepatiwa mafunzo na ushauri juu ya kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, ikiwa ni pamoja na kupewa uwezo wa kisheria kupitia dirisha la upashanaji habari la wanawake mkoani hapa.
Hayo yamesemwa na Ofisa wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wa Manispaa ya Morogoro, Monica Lindi wakati alipokuwa anasoma risala katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Jamhuri, mkoani hapa.
Lindi alisema kuwa Halmashauri katika manispaa ya Morogoro wameamua kuwa na dirisha la upashanaji habari la wanawake ambalo litawasaidia wanawake kupatiwa ushauri ikiwa ni pamoja na ufadhili hivyo kujiendeleza na kujikwamua kiuchumi.
Aidha alisema kuwa pamoja na mafanikio walioyapata lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama upungufu wa mabweni na hosteli kwa watoto wa kike katika shule za serikali katika manispaa hiyo.
Changamoto nyingine ni jamii kukosa hamasa za kuchangia katika elimu hasa kwa watoto wa kike na kuchangia shughuli za sherehe na hivyo kuacha jukumu la kumwendeleza mtoto wa kike kwa wafadhili na serikali.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Halima Dendegu akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa alisema kuwa jamii inapaswa kutambua umuhimu wa kuwawezesha wasichana kupata elimu bora ambayo itawawezesha kupata ajira na hivyo kuongeza kipato kwa jamii na taifa kwa ujumla
No comments:
Post a Comment