Pages

Wednesday 14 March 2012

TBL YAIPATIA HOSPITALI YA MOROGORO, SHULE ZA SEKONDARI 12 ZAPATA MSAADA WA SH51.6 MILIONI.


SHULE  12 za sekondari zilizoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na hospitali ya mkoa, zimepeta msaada wa Sh51.6 kwa ajili ya kuziwezesha kuchimba visima, kuweka matangi ya kuhifadhia maji na dawa katika  shule hizo. Fedha hizo zimetolewa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) chini ya mkakati wake wa kuboresha huduma za maji katika taasisi mbalimbali.


Akikabidhi fedha hizo juzi, Mkurugenzi wa Uhusiano na Sheria wa TBL, Steven Kilindo, alisema Sh24.9 milioni katika fedha hizo ni kwa ajili ya hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Alisema kampuni hiyo imekuwa ikitumia sehemu ya pato lake, kuiwezesha jamii kuondokana na kero ya kukosa  huduma za maji.


Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hospitali ya mkoani hapa, Kaimu Mganga Mkuu, Anthon Mwakibete, alisema fedha hizo zitasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la maji katika hospitali hiyo.

 “Hapa hospitalini kuna wakati tulikabiliwa na tatizo la maji kwa takribani siku mbili. Kwa kweli ilikuwa ni shida kubwa kwa sababu maji yanahitajika wakati wote katika uendeshaji wa shughuli za hospitali,”alisema Mwakibete.


Ofisa Afya wa Mkoa wa Morogoro, Carl Lyimo, alisisitizia umuhimu wa kuchimba visima katika maeneo salama ili maji yatakayopatikana yaweze salama na kwa matumizi ya wagonjwa na shughuli nyingine za hospitali.


Kampuni ya Bia Tanzania pia ilikabidhi Sh26.7 milioni kwa uongozi wa Manispaa ya Morogoro, ili kugharimia uwekaji wa matangi ya maji na dawa katika shule 12 za sekondari ya manispaa hiyo.

Shule zitakazonufaika na msaada huo ni Bondwa, Bungodimwe, Kingo, Kola Hill, Mjimpya, Mgulasi, Uluguru, Uhuru, Nanenane, Tubuyu, Mafisa na Tushikamane ambazo ni shule za  kata.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo, alisema msaada huo ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa shule nyingi katika Manispaa ya Morogoro, hazina huduma za maji.

Nondo alisema hata hivyo manispaa imekuwa ikijitahidi kuboresha huduma za maji na kwamba hivi karibuni, imepima viwanja katika maeneo ya Kiegeya A na B, Kipera, Kasanga na Mbunge kwa ajili ya uchimbaji wa visima virefu.

No comments: