Pages

Sunday 1 April 2012

MOROGORO YAPEWA SHILINGI MIL 159/- ZA MAJI.


HALMASHAURI za wilaya za Mkoa wa Morogoro kwa mwaka huu wa fedha, zimepokea Sh milioni 159.7 na kuzitumia katika utekelezaji wa miradi ya maji inayoleta matokeo ya haraka. 

Pia sekta ya maji imeanza kutekeleza miradi miwili ya maji kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) na Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC). 

Miradi hiyo ya MCC inatekelezwa katika Manispaa ya Morogoro, Miji Midogo ya Kilosa, Gairo, Mvomero, Turiani, Mikumo na Mahenge. 

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro, Lameck Noah alisema hayo hivi karibuni mjini hapa katika mkutano wa wadau wa sekta mbalimbali, ambao walihoji juu ya mkakati wa Serikali wa kuwapatia maji safi na salama bila matatizo. 

Alitaja idadi ya watu wanaopata maji safi na salama vijijini kuwa ni 1,044,478 sawa na asilimia 62.95 na malengo ya kitaifa ya utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi waishio vijijini ilitakiwa hadi mwaka 2010 iwe imefikia asilimia 65. 

Mbali na maeneo ya vijijini, huduma ya upatikanaji wa maji mjini kimkoa imefikia watu 178,309 sawa na asilimia 93 na hivyo kuvuka malengo yaliyowekwa hadi mwaka 2010 ambayo ni asilimia 90. 

Akizungumzia sekta ya ushirika na masoko, Noah alisema mkoa huo una Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) 331 vyenye mtaji mkubwa ambapo wanachama wake wamefikia 45,127; kati ya hao wanaume ni 25,869 na wanawake ni 19,258. 

Alisema hadi Agosti mwaka jana, Saccos hizo zilikuwa zimetoa mikopo kwa wanachama yenye thamani ya Sh milioni 33.3 na marejesho ya Sh 22.9.

Source: Habari Leo

No comments: