Pages

Monday, 2 April 2012

CHUPA TUPU ZAWA DILI MOROGORO.

Mjasiriamali Prudence Kayusi akiwa katika kituo chake cha biashara ya chupa tupu eneo la Sabasaba, Manispaa ya Morogoro.
---
WAHENGA walisema “Binadamu haishi kwa kutegemea mkate pekee”. 
Huo ni msemo waliotumia ili kusisitiza umuhimu wa kujitafutia riziki kwa kufanya kazi halali ya kujipatia kipato. Kutokana na hali hiyo, siku zote binadamu amejiwekea utaratibu wa kujishughulisha, kwa kazi za kujiajiri mwenyewe au kuajiriwa, kama vile ofisini, zote kwa lengo kuu moja la kuboresha maisha. 


Mwandishi wa makala haya, amefanya utafiti kwa muda sasa juu ya shughuli ya kuokota chupa tupu za plastiki, ambazo tayari watu wamekunywa maji na kuzitupa, wanunuzi wa kati na wakubwa wa bidhaa hiyo na faida wanayoipata wajasiriamali waliojikita kwenye biashara hiyo. 

Zamani chupa hizo, baada ya kilichomo ndani yake kutumiwa, zilikuwa ama zikitupwa jalalani au kando ya barabara. Wakati mwingine ziliachwa ovyo kila kona, hivyo kuwa ni sehemu ya uchafu. 

Lakini, maendeleo ya sayansi na teknolojia, yaliyochangiwa na utandawazi, yameleta mabadiliko, kwani chupa hizo polepole zikaanza kutafutwa na watu wachache na haikujulikana zinahitajika kwa ajili ya nini na kwa manufaa gani. 

Kwa Manispaa ya Morogoro, mtu wa kwanza kujitosa katika ukusanyaji wa chupa hizo kupitia vijana aliowateua, alikuwa ni Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka, maarufu kama ‘ SMG’. 

Cheka alianzisha biashara ya kununua chupa za maji safi mitaani; na hatimaye alikwenda kuwauzia wafanyabiashara wakubwa wa Kichina waliopo hapa nchini. Wakati huo, bondia huyo maarufu nchini, alisema amelazimika kuanza biashara hiyo, baada ya kubaini kwamba mchezo wa ngumi ni wa msimu na unaohitaji uwe na kazi ya ziada ya kufanya. 

Anasema aliamua kufanya kazi hiyo ya ujasiriamali ili kufidia pengo la mahitaji ya fedha, katika muda anapokaa bure bila kucheza pambano la ngumi. Wakati huo aliwapata vijana 10, waliokuwa wakifanya kazi hiyo. 

Alikodisha sehemu ya dampo la Manispaa, kwa ajili ya kuhifadhi chupa zake kabla ya kujisafirisha kupeleka kwa wateja wake, ambao ni wachina wa Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa bondia huyo, chupa tupu za maji alizokusanya mitaani kila mwezi, zilikuwa na zaidi ya kilo 1,500 hadi 2,000 na mara baada ya kuzikusanya, alizisafirisha kwa magari ya kukodi hadi Dar es Salaam ili kuwauzia wafanyabiashara hao wa Kichina. 

“Kwa wastani, tani mbili za chupa hizi, ziliweza kunipatia shilingi 400,000 hadi shilingi 500,000. Lakini, ukiondoa gharama zote, ninapata faida kidogo, inayoniwezesha kujikimu 
kimaisha”, anasema Cheka. 

Mbali na Cheka, wapo wafanyabiashara wengi wanaume na wanawake katika Manispaa ya Morogoro, ambao wamejitokeza kukusanya chupa hizo na kuzisafirisha hadi kwenye masoko makubwa ya Dar es Salaam. 

Miongoni mwa wafanyabiashara hao ni Prudence Kayusi, ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam. Yeye ameamua kuweka makazi yake katika Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuendesha shughuli hiyo. 

Akihojiwa na mwandishi wa makala haya, anasema kazi hiyo ni sawa na nyinginezo na kwamba imekuwa ikimwingizia kipato cha kuishi yeye na familia yake. Anasema, kabla ya kuwapata waokotaji wa chupa hizo kutoka mitaani, alikuwa akiifanya mwenyewe kazi hiyo. 

Anasema wakati huo, baadhi ya watu walimwona kama ni mwendawazimu. “Nilianza kazi hii mwaka jana mwezi wa nane. Nilikuwa nikiokota chupa mimi mwenyewe kwa mikono yangu jalalani, mabaa na kumbi za harusi. 

Baadaye nikafanikiwa kuongeza mtaji wangu, ukawa mkubwa, kiasi kilichoniwezesha kununua kutoka kwa vijana wa mitaani na wengine kuniletea kwenye eneo langu”, anasema Kayusi. Anasema, katika biashara hiyo, kuna makambuni mengi hasa ya Kichina yanayonunua bidhaa hizo, ambapo huzisafisha na kuzitoa lebo na kuzisafirisha nje ya nchi. 

Chupa zingine huzisaga na kusafirisha kama malighafi, kwenda katika viwanda vya kwao kutengeneza bidhaa mbalimbali. Anasema, katika Jiji la Dar es Salaam, biashara hiyo imeshamiri na ina ushindani mkubwa, hivyo kutokana na mtaji wake kuwa mdogo, 
ameamua kuweka makazi yake mkoani Morogoro, kwa kuwa malighafi hiyo ipo ya kutosha. 

“Chupa kilo moja ni shilingi 300 hadi shilingi 550…wakusanyaji wanaweza kuleta hapa kwangu kilo za kutosha, ninaweza kumlipa mtu hadi shilingi 4,500 kwa mzigo aliouleta, na si mtu mmoja, bali ni wengi wanaleta kwa siku,” anasema mjasiriamali huyo. 

Anaongeza “Siku zote ‘Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe’, hivyo wajasiriamali wadogo wanaookota mitaani chupa hizi, wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu hiyo”, anasema Kayusi. 

Kwa upande wake, mjasiriamali wa biashara hiyo, Ramadhan Hussein anasema siku za nyuma chupa tupu za maji zilikuwa zikizagaa na kuonekana ni uchafu. Lakini, hivi sasa chupa tupu ni bidhaa adimu ; na kila kona inapoonekana, huokotwa na vijana, hasa wanaoshi kwenye mazingira hatarishi . 

“Vijana wengi hasa wanaoitwa wa mitaani, ndiyo walijikikita na kazi ya kuokota chupa kila kona …na wakija hapa tunawapimia mizigo yao na kuwapatia fedha, ambazo wanazitumia kwa kula chakula kwa akina mama lishe. 

Kuwepo kwa biashara ya chupa tupu za plastiki, kumewakomboa watu wengi. Jambo la msingi ni kuwa ni lazima usafi wa chupa, uzingatiwe na ziwekwe kwenye maeneo yenye mazingira mazuri na si jalalani tena “, anasema Hussein. 

Hata hivyo, anasema, siyo watoto wa mitaani tu ndiyo wenye hali duni ya kimaisha, bali hata wanaume nao wamejitosa kuokota chupa hicho na kuwapekelea wanunuzi. Wamefanya 
hivyo baada ya kutambua kuwa fedha za biashara hiyo, zipo nje nje. 

Nao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro, waliozungumza kwa nyakati tofauti kuhusu biashara hiyo, wanasema imewezesha na kuzifanya chupa hizo kuwa adimu. Wanasema zamani chupa hizo zilikuwa ni kero, kutokana na kuzagaa ovyo, lakini sasa ni nadra kuzikuta 
mitaani. 

Hata hivyo, wamesema, uchafu uliopo hivi sasa ni wa takataka za aina nyingine; na si chupa hizo, ambazo sasa ni ‘dili’ la kuwapatia kipato wananchi wenye kipato duni katika kaya.

Source: Habari Leo

No comments: