Pages

Friday, 6 April 2012

UJENZI WA DARAJA LA MTO SANGASANGA WALETA FARAJA GEZAULOLE.


UJENZI wa daraja la Mto Sangasanga linalounganisha Kitongoji cha Gezaulole katika Barabara ya Gwata Ujembe, Kata ya Gwata, Tarafa ya Mikese, Wilaya ya Morogoro litakalowaondolea adha wananchi wa pande mbili hizo kutokana na hofu ya kupoteza maisha yao, litagharimu kiasi cha Sh milioni 32. 

Wananchi wa Kitongoji hicho na wale wa Gwata Ujembe, kwa muda mrefu wamekuwa na hofu 
baada ya miaka ya nyuma kuwepo matukio ya watu kufa baada ya kusombwa na maji wakati 
walipoamua kupita mtoni kutokana na ukosefu wa daraja. 

Daraja hilo lilianza kujengwa Agosti 18, mwaka jana fedha yake hiyo imetolewa na TASAF na pia mradi huo, umelenga kuchimbwa kwa barabara yenye urefu wa kilometa 4.2 ili kuwezesha kurahisisha usafiri mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo Aprili mwaka huu. 

Mwenyekiti wa Mradi huo, Rehema Kisimikwe alisema Mradi huo uliobuniwa na wananchi wa 
Kitongoji cha Gezaulole kutokana na adha walizokuwa wakizipata hasa kwa wanafunzi kukwama kwenda shule na wananchi wengine kushindwa kwenda kujipatia mahitaji muhimu sehemu mbalimbali nje ya Kitongoji hicho. 

Alisema ukosefu wa daraja umeendelea kuleta adha kwa wananchi wa pande mbili zilizotenganishwa na mto huo hasa wakati wa mvua za masika mto unapojaa maji na kusababisha mafuriko yanayowafanya wananchi washindwe kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine wakiwemo na wanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari. 

Naye Katibu wa Mradi huo, Yusuph Chuma, alisema miaka ya hivi karibuni Mto huo ulisababisha vifo vya watu wawili kusombwa na maji ya mafuriko,na kusisitiza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutatoa ahueni kwa wananchi na ni ukombozi wao katika maendeleo.

No comments: