KUKOSEKANA kwa ajira za vijana kumetajwa kuwa moja ya sababu za kundi hilo kujiingiza katika makundi mabaya ikiwamo yanatoteleza mauji ya vikongwe hasa wanawake nchini.
Mwenyekiti mtendaji wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Consern For The Elderly Tanzania (COEL) Jamaton Magodi alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mwezi mmoja ya ujasiriamali, Usindikaji na uandishi wa habari kwa wanachama wa shirika hilo kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro na Kagera yanayoendelea mjini Morogoro ambapo alisema kuwa ajira ni muhimu kwa vijana kwa kuwa wao ndiyo tegemeo la taifa.
Alisema kuwa mauaji ya vikongwe yanatokana na sababu mbalimbali zikiwamo mazingira mabovu ya malezi yasiyozingatia maadili ya taifa, kukosekana kwa ajira na rushwa na kuiomba Serikali kushirikiana na shirika hilo katika kutoa elimu kwa wanajamii maeneo mbalimbali nchini kuhusu maadili mema.
Magodi alisema kuwa tangu mwaka 2004 COEL ilipoanzishwa hadi 2011 jumla ya wanawake vikongwe 24,000 wameuawa kikatili nchini huku ukatili huo ukionekana kukithiri zaidi mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Shinyanga,Tabora, Mwanza na Musoma huku shirika lake likifika mikoa 17 sasa.
“Mauaji hayo yanatokana na wanannchi wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha, ujinga, rushwa na hata macho kuwa mekundu kwa wazee wetu. Mauaji hayo ni dhambi ,”alisema Magodi.
Alibainisha kuwa shirika lake limekuwa na jukumu la kuelimisha jamii kuondokana na maovu katika maeneo yao na kuhakikisha wanakuwa na maadili mema.
Mgeni rasmi katika mafunzo hayo Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro Dk Isack Kama alilipongeza shirika la COEL kwa ushirikiano wake na Serikali katika kuelimisha jamii mambo mbalimbali na kukemea uovu.
Dk Kama alisema kuwa Serikali imekuwa ikisaidia mashirika yanayojishughulisha na utoaji elimu kwa jamii katika kukemea maovu ili kuwa na taifa lenye uadilifu na mwelekeo mwema akiwataka wanachama wa shirika hilo kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili kupata misaada na mikopo kuotka serikalini.
No comments:
Post a Comment